
Siku ya Jana katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kulipigwa mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga katika mchezo wa Ligi kuu nchini Tanzania maarufu kama NBC premier league.
Yanga waliingia katika mchezo huo wakiwa wanaongoza Ligi huku watani wao Simba wakishika nafasi ya pili.
Mchezo ulianza kwa kasi na timu zote zikicheza kwa tahadhari na nidhamu ili kutoruhusu kufungwa goli la mapema.kwa dakika 45 za kipindi cha Kwanza hakukuwa na shuti lililopigwa golini kwa kipa wa Simba au wa Yanga.
Kipindi cha pili timu zilianza kufunguka na kutengeneza nafasi za kufunga na Simba ndo waliofanikiwa kufika langoni mwa Yanga Mara nyingi zaidi ila uimara wa golikipa Diarra na mabeki wake Mwamnyeto na Dickson Job walihakikisha wavu hauguswi.
Hadi dakika 90 za mwamuzi Eli Sasii zinakamilika sio Simba au Yanga waliofanikiwa kupata bao.
Licha ya mechi kuisha kwa suluhu pacha, mchezo wa Jana ulikua miongoni mwa michezo Bora kiufundi kuchezwa kati ya Simba na Yanga kwa miaka ya hivi karibuni. Khalid Aucho, Yannick Bangala na Feisal Salum wa Yanga pamoja na Jonas Mkude, Sadio Kanoute wa Simba walitupa mpambano mkali katikati mwa uwanja.
Hivyo mtanange wa Jana unazidi kuipa heshima dabi hii ya Kariakoo na kuendelea kuifanya kuwa miongoni mwa dabi Bora barani Afrika.
Vita inaendelea na tutajua Nani atafanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi ifikapo mwezi Mei mwakani je Yanga wakafanikiwa kuhitimisha utawala wa Simba, au Simba wataendeleza ubabe wao na kubeba ubingwa kwa Mara ya Tano mfululizo, ama tutapata bingwa mwingine Azam, polisi , ruvu shooting, Namungo?
